Mahakama yaikataa ripoti ya video ya uhaini ya Lissu

-rickmedia: Saraphina Jerry

Saraphina Jerry

4 hours ago
rickmedia: mahakama-yaikataa-ripoti-video-uhaini-lissu-885-rickmedia

Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam, imeikataa ripoti ya uchunguzi wa uhalisia wa picha mjongeo (video clip) ya Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, anayekabiliwa na kesi ya uhaini, yenye maudhui yanayodaiwa kuwa ya uhaini.

Upande wa mashtaka katika kesi hiyo jana Jumatano, Oktoba 22, 2025 kupitia shahidi wake wa tatu iliiomba mahakama iipokee ripoti hiyo kuwa kielelezo cha ushahidi wa upande wa mashtaka.

Hata hivyo, Lissu aliweka pingamizi dhidi ya ripoti hiyo isipokewe akidai shahidi huyo hana mamlaka ya kisheria kuiwasilisha mahakamani wala kuiandaa ripoti hiyo kwa kuwa si mtaalamu wa uhalifu wa kimtandao.

Licha ya upande wa mashtaka kupinga hoja zake kuwa hazina mashiko kisheria, lakini Mahakama katika uamuzi wake leo Alhamisi Oktoba 23, 2025 imekubaliana na pingamizi lake baada ya kuridhia na hoja zake, hivyo ikaikataa ripoti hiyo ikieleza kuwa shahidi huyo hana mamlaka ya kisheria kuwasilisha ripoti hiyo kwa kuwa si mtaalamu wa masuala ya uhalifu mtandao.