Mahakama ya Rufaa ya Tanzania imetupilia mbali Rufaa iliyokatwa na Upande wa Jamhuri, ikipinga uamuzi uliotolewa na Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Arusha, kumuachilia huru aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya na wenzake wawili (Sylvester Nyegu na Daniel Mbura) waliokuwa wamehukumiwa Kifungo cha miaka 30 jela.
Mahakama imesema imejiridhisha kwa ushahidi usioacha mashaka kuwa wajibu Rufaa (Sabaya na Wenzake) hawakuthibitika kutenda kosa la Unyang’anyi wa kutumia Silaha au Makundi bali walikuwa katika majukumu halali ya kufuatilia Makosa ya Uhujumu Uchumi.
Awali, Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) alikata rufaa katika Mahakama hiyo akipinga uamuzi uliowaachia huru Watuhumiwa akidai walihusika na uhalifu wa Kutumia Silaha na Kuendesha Genge la Uporaji.