Serikali ya Taliban imepiga marufuku vitabu vyote vilivyoandikwa na wanawake katika vyuo vikuu nchini Afghanistan. Kati ya vitabu 680 vilivyopitiwa, takriban vitabu 140 vimeondolewa rasmi kwa madai ya kukinzana na mafundisho ya Sharia na sera za utawala huo.
Aidha, amri hiyo mpya inahusisha pia marufuku ya masomo 18 ambayo hayajaainishwa rasmi, ikiwa ni mwendelezo wa vikwazo vya elimu vilivyowekwa dhidi ya wanawake na wasichana tangu kundi hilo liliporejea madarakani miaka minne iliyopita.
Hatua hii imeibua wasiwasi mkubwa ndani na nje ya Afghanistan, huku wadau wa elimu na haki za binadamu wakielezea hofu yao juu ya mustakabali wa elimu kwa wanawake chini ya utawala wa Taliban.
Tangu kurejea kwao madarakani mwaka 2021, Taliban wamekuwa wakikumbana na ukosoaji mkali kimataifa kutokana na sera zao zinazowabagua wanawake, hasa katika sekta ya elimu na ajira.