Mchezaji maarufu wa kandanda, Cristiano Ronaldo amejiita "mchezaji kamili zaidi katika historia ya kandanda."
Superstaa huyu wa Kireno alizungumza katika mahojiano ya hivi karibuni na Edu Aguirre, mwandishi wa habari kutoka ‘El Chiringuito’.
Alipoulizwa kama anaamini yeye ni mchezaji bora zaidi katika historia, Ronaldo alikubali kwamba mashabiki wanaweza kumpendelea Lionel Messi, Pele, na Diego Maradona, lakini alijitangaza kama mchezaji kamili zaidi katika historia.
"Nadhani mimi ni mchezaji kamili zaidi ambaye amewahi kuwapo. Watu wanaweza kumpenda Messi, Maradona au Pele, na mimi niwaheshimu, lakini mimi ni mchezaji kamili zaidi. Mimi ndiye mchezaji bora katika historia ya kandanda. Sijawahi kuona mtu bora kuliko mimi katika historia ya kandanda na nasema ukweli kutoka moyoni mwangu."
Ronaldo, ambaye anachezea klabu ya Al-Nassr katika Ligi ya Pro ya Saudi Arabia (SPL), amezoa tuzo tano za Ballon d'Or katika kariya yake pamoja na mataji kadhaa ikiwa ni pamoja na Ligi ya Mabingwa, Ligi Kuu ya Uingereza, La Liga, na Serie A.
Kombe la Dunia la FIFA linabaki kuwa heshima kuu pekee isiyokuwepo katika kabati lake la tuzo. Aliwahi kushinda Euro 2016 na Ligi ya Mataifa ya 2019 akiwa na Ureno, akiongoza timu yake katika mashindano hayo yote.